Friday, 6 November 2015

ICC YATAKA KUKABIDHIWA SEIFUL ISLAM GADDAFI

 
 Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi imeitaka serikali ya Libya yenye makao yake Tripoli imkabidhi kwa mahakama hiyo Saiful Islam Gaddafi mwana wa kiume wa dikteta wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi. 
Saiful Islam Gaddafi alikuwa amekatiwa hukumu ya kunyongwa na mahakama moja ya Tripoli. Bi Fatou Bensouda Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC amesema katika ripoti aliyoiwasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, pamoja na kuwa mahakama hiyo ilishawaomba rasmi kwa mara kadhaa viongozi wa Tripoli  ili wamkabidhi Saiful Islam Gaddafi kwa mahakama ya jinai ya ICC, lakini serikali ya Libya imekuwa ikipinga maombi  hayo.
 
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mwaka 2011 ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni Saiful Islam Gaddafi  kutokana na jinai dhidi ya binadamu alizotenda huko Libya. 

Mahakama ya Rufaa ya Tripoli mwishoni mwa mwezi Julai mwaka jana iliwahukumu kunyongwa shakhsia kumi wa utawala wa zamani wa Libya akiwemo mwana huyo wa Muammar Gaddafi baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wafanya maandamano,  kuasisi makundi ya kukandamiza mapinduzi ya wananchi katika matukio ya Februari 17 Februari mwaka 2011 na pia kuhusika katika ufisadi nchini. 

No comments:

Post a Comment